Add parallel Print Page Options

Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao

(Mt 24:1-14; Mk 13:1-13)

Baadhi ya watu walikuwa wanazungumza kuhusu uzuri wa Hekalu lililojengwa kwa mawe safi na kupambwa kutokana na matoleo mbalimbali ambayo watu humtolea Mungu ili kutimiza nadhili zao.

Lakini Yesu akasema, “Wakati utafika ambao yote mnayoyaona hapa yatateketezwa. Kila jiwe katika majengo haya litatupwa chini. Hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jingine.”

Baadhi ya watu wakamwuliza Yesu, “Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Dalili ipi itatuonyesha kwamba ni wakati wa mambo haya kutokea?”

Yesu akasema, “Iweni waangalifu, msije mkarubuniwa. Watu wengi watakuja wakitumia jina langu, watasema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[a] na ‘Wakati sahihi umefika!’ Lakini msiwafuate. Mtakaposikia kuhusu vita na machafuko, msiogope. Mambo haya lazima yatokee kwanza. Lakini mwisho hautakuja haraka.”

10 Kisha Yesu akawaambia, “Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. 11 Kutakuwa matetemeko makubwa, kutakuwa njaa na magonjwa ya kutisha sehemu nyingi. Mambo ya kutisha yatatokea, na mambo ya kushangaza yatatokea kutoka mbinguni ili kuwaonya watu.

12 Lakini kabla ya mambo haya yote kutokea, watu watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawahukumu katika masinagogi yao na kuwafunga gerezani. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na magavana. Watawatendea mambo haya yote kwa sababu ninyi ni wafuasi wangu. 13 Lakini hili litawapa ninyi fursa ya kuhubiri juu yangu. 14 Msihofu namna mtakavyojitetea, 15 Nitawapa hekima kusema mambo ambayo adui zenu watashindwa kuyajibu. 16 Hata wazazi wenu, ndugu zenu, jamaa, na marafiki watawageuka. Watawaua baadhi yenu. 17 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. 18 Lakini hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea. 19 Mtayaokoa maisha yenu ikiwa mtaendelea kuwa imara katika imani mnapopita katika mambo haya yote.

Kuharibiwa Kwa Mji wa Yerusalemu

(Mt 24:15-21; Mk 13:14-19)

20 Mtakapoona majeshi yameuzunguka mji wa Yerusalemu, ndipo mtajua kuwa wakati wa kuharibiwa kwake umefika. 21 Watu walioko katika Uyahudi wakati huo wakimbilie milimani. Mtu yeyote atakaye kuwa Yerusalemu wakati huo aondoke haraka. Ikiwa utakuwa karibu na mji, usiingie mjini! 22 Manabii waliandika mambo mengi kuhusu wakati ambao Mungu atawaadhibu watu wake. Wakati ninaouzungumzia ni wakati ambao mambo haya yote lazima yatokee. 23 Wakati huu utakuwa mgumu kwa wanawake wenye mimba au wanaonyonyesha watoto wadogo, kwa sababu mambo mabaya yatakuja katika nchi hii. Mungu atawaadhibu watu wake kwa sababu wamemkasirisha. 24 Baadhi ya watu watauawa, wengine watafanywa watumwa na kuchukuliwa katika nchi mbalimbali. Mji mtakatifu wa Yerusalemu utatekwa na kuwekwa chini ya utawala wa wageni mpaka wakati ulioruhusiwa wao kufanya hivi utakapokwisha.

Read full chapter

Footnotes

  1. 21:8 Masihi Kwa maana ya kawaida, “Yule ambaye”, kwa maana ya Mfalme Mteule wa Mungu aliyetumwa na Mungu. Tazama Mt 24:5 na Masihi katika Orodha ya Maneno.