Add parallel Print Page Options

Njiani Kwenda Emausi

(Mk 16:12-13)

13 Siku hiyo hiyo, wafuasi wawili[a] wa Yesu walikuwa wanakwenda kwenye mji mdogo uitwao Emausi, uliokuwa yapata kilomita kumi na mbili[b] kutoka Yerusalemu. 14 Walikuwa wanazungumza kuhusu mambo yote yaliyotokea. 15 Walipokuwa wakizungumza, wakijadiliana juu ya mambo haya, Yesu mwenyewe aliwasogelea na akawa anatembea nao. 16 Lakini hawakuruhusiwa kumtambua. 17 Yesu akawauliza, “Ni mambo gani ninayosikia mnajadiliana mnapotembea?”

Wale wafuasi wawili wakasimama, sura zao zilionekana zenye huzuni. 18 Mmoja wao, aliyeitwa Kleopa akasema, “Lazima wewe ni mtu pekee katika Yerusalemu ambaye hujui yaliyotokea huko.”

19 Yesu akasema, “Unasema kuhusu nini?”

Wakasema, “Ni kuhusu Yesu, kutoka Nazareti, alikuwa nabii mkuu mbele za Mungu na watu wote. Alisema na kutenda mambo makuu mengi. 20 Lakini viongozi wetu na viongozi wa makuhani walimtoa ili ahukumiwe na kuuawa. Wakampigilia msalabani. 21 Tulitegemea kuwa ndiye atakayeiweka huru Israeli. Lakini sasa haya yote yametokea.

Na sasa kitu kingine: Imekuwa ni siku tatu tangu alipouawa, 22 lakini leo baadhi ya wanawake kutoka kwenye kundi letu walituambia jambo la kushangaza. Mapema asubuhi hii walikwenda kaburini ambako mwili wa Yesu ulilazwa. 23 Lakini hawakuuona mwili wake pale. Walikuja na kutuambia kuwa wamewaona malaika. Malaika waliwaambia Yesu yu hai! 24 Hivyo baadhi ya watu walio katika kundi letu walikwenda kaburini pia. Ilikuwa kama wanawake walivyosema. Waliliona kaburi, lakini hawakumwona Yesu.”

25 Ndipo Yesu akawaambia, “Ninyi ni wajinga na wazito wa kuyakubali yale waliyoandika manabii. 26 Manabii waliandika kwamba Masihi lazima ateseke kwa mambo haya kabla hajaingia katika utukufu wa ufalme wake.” 27 Kisha akaanza kufafanua kila kitu walichosema manabii kuhusu yeye. Alianzia katika vitabu vya Musa na kusema yale waliyosema manabii kuhusu yeye.

28 Wakakaribia mji wa Emausi, na Yesu akafanya kama vile alikuwa anaendelea mbele. 29 Lakini walimtaka akae, wakamsihi: “Kaa nasi. Tayari ni usiku. Mchana unakaribia kwisha.” Hivyo aliingia ndani kukaa nao.

30 Alipokuwa mezani pamoja nao ili kula chakula cha usiku, Yesu akachukua mkate na kushukuru. Kisha akaumega na kuwapa. 31 Baada ya kufanya hivyo, wafuasi wale wawili wakaruhusiwa kumtambua. Lakini walipojua yeye ni nani, alitoweka. 32 Wakasemezana, “Alivyokuwa anazungumza nasi tulipokuwa barabarani, tulijisikia kama moto unawaka ndani yetu. Ilitusisimua sana alipotufafanulia maana halisi ya Maandiko!”

33 Hivyo wafuasi wale wawili wa Bwana Yesu wakasimama na kurudi Yerusalemu haraka. Walipofika Yerusalemu waliwakuta mitume kumi na mmoja wamekusanyika pamoja na wafuasi wengine wa Bwana Yesu. 34 Kundi likawaambia wale wafuasi wawili, “Hakika Bwana amefufuka kutoka kwa wafu! Alimtokea Simoni.”

35 Ndipo wafuasi wawili wakaeleza kilichotokea barabarani. Wakaeleza jinsi walivyomtambua Yesu aliposhiriki mkate pamoja nao.

Read full chapter

Footnotes

  1. 24:13 wafuasi wawili Kwa maana ya kawaida, “Miongoni mwa wafuasi”. Ni wazi kutokana na simulizi kuwa wote wawili ni wafuasi wa Yesu, lakini mmoja wao tu ndiye anayetajwa jina (mstari wa 18). Inawezekana akawa ndiye Kleopa, anayeelezwa katika Yh 19:25 kama mume wa mmoja wa wanawake anayeitwa Mariamu. Inawezekama mfuasi wa pili anayezungumzwa hapa ndiye huyu Mariamu.
  2. 24:13 kilomita kumi na mbili Kwa Kiyunani umbali huo ni sawa na “stadia 60”.