Add parallel Print Page Options

Yohana Atuma Watu Kumwuliza Yesu Swali

(Mt 11:2-19)

18 Wafuasi wa Yohana Mbatizaji walimweleza Yohana Mbatizaji kuhusu mambo haya yote. Naye aliwaita wanafunzi wake wawili. 19 Akawatuma waende na kumwuliza Yesu, “Wewe ndiye tuliyesikia anakuja, au tumsubiri mwingine?”

20 Wafuasi wa Yohana walipofika kwa Yesu, wakasema, “Yohana Mbatizaji ametutuma kwako tukuulize: ‘Wewe ndiye yule ajaye, au tumsubiri mwingine?’”

21 Wakati ule ule Yesu alikuwa amewaponya watu wengi madhaifu na magonjwa yao. Aliwaponya waliokuwa na pepo wabaya na kuwafanya wasiyeona wengi kuona. 22 Kisha aliwaambia wanafunzi wa Yohana, “Nendeni mkamweleze Yohana yale mliyoyaona na kuyasikia: wasiyeona wanaona, walemavu wa miguu wanatembea, wenye magonjwa mabaya ya ngozi wanatakasika, wasiyesikia wanasikia. Waliokufa wanafufuliwa na Habari Njema inahubiriwa kwa maskini. 23 Heri wale wasio na mashaka kunikubali mimi.”[a]

24 Baada ya wanafunzi wa Yohana kuondoka, Yesu akaanza kuwaambia watu kuhusu Yohana, “Mlitoka kwenda jangwani kuona nini? Mtu aliyekuwa dhaifu, kama unyasi unaotikiswa na upepo? 25 Mlitegemea kuona nini? Mtu aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hilo. Watu wanaovaa mavazi mazuri na kuishi kwa anasa wako katika majumba ya wafalme. 26 Sasa, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yohana ni zaidi ya nabii. 27 Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:

‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
    Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’(A)

28 Ninawaambia, hakuna aliyewahi kuzaliwa aliye mkuu kuliko Yohana. Lakini mwenye umuhimu mdogo, katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.”

29 (Watu waliposikia hili, wote walikubali kuwa mafundisho ya Mungu yalikuwa mazuri. Hata watoza ushuru waliobatizwa na Yohana walikiri. 30 Lakini Mafarisayo na wanasheria walikataa kuukubali mpango wa Mungu kwa ajili yao; hawakumruhusu Yohana awabatize.)

31 “Niseme nini kuhusu watu wa wakati huu? Niwafananishe na nini? Wanafanana na nini? 32 Ni kama watoto waliokaa sokoni. Kundi moja la watoto likawaita watoto wengine na kusema,

‘Tuliwapigia filimbi
    lakini hamkucheza.
Tuliwaimba wimbo wa huzuni,
    lakini hamkulia.’

33 Yohana Mbatizaji alikuja na hakula chakula cha kawaida au kunywa divai. Nanyi mkasema, ‘Ana pepo ndani yake.’ 34 Mwana wa Adamu amekuja anakula na kunywa. Mnasema, ‘Mwangalieni anakula sana na kunywa sana divai. Ni rafiki wa watoza ushuru na watenda dhambi wengine.’ 35 Lakini hekima huoneshwa kuwa sahihi kwa wale wanaoikubali.”

Read full chapter

Footnotes

  1. 7:23 Heri … kunikubali mimi Au “Baraka kuu ni kwa wale wasio na mashaka kunikubali.”