Add parallel Print Page Options

29 Mara baada ya mateso ya siku hizo, mambo haya yatatokea:

‘Jua litakuwa jeusi,
    na mwezi hautatoa mwanga.
Nyota zitaanguka kutoka angani,
    na kila kitu kilicho angani
    kitatikiswa kutoka mahali pake.’[a]

30 Kisha kutatokea ishara angani kuwa Mwana wa Adamu anakuja. Watu wote wa ulimwengu watajipiga kifuani wakiomboleza. Kila mtu atamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani akiwa na nguvu na utukufu mkuu. 31 Naye atatumia parapanda kuu kuwatuma malaika zake kila mahali duniani. Nao watawakusanya wateule wake kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine.

32 Jifunze kwa mtini: Matawi yake yanapokuwa ya kijani na laini na kuanza kutoa majani mapya, ndipo mnatambua kuwa majira ya joto yamekaribia. 33 Katika namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yakitokea, mtajua kuwa wakati[b] umekaribia wa kile kitakachotokea. 34 Ninawahakikishia kuwa mambo haya yote yatatokea wakati ambao baadhi ya watu wa nyakati hizi wakiwa bado hai. 35 Ulimwengu wote, dunia na anga vitaangamizwa, lakini maneno yangu yatadumu milele.

Mungu Peke Yake Ndiye Ajuaye Siku ya Kurudi kwa Mwana wa Adamu

(Mk 13:32,35; Lk 17:26-30,34-36)

36 Hakuna anayeijua siku wala wakati. Malaika wa mbinguni hawaijui hata Mwana hajui itakuwa lini. Baba peke yake ndiye anayejua.

37 Mwana wa Adamu atakapokuja, itakuwa kama ilivyokuwa nyakati za Nuhu. 38 Siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuwatoa binti zao kuolewa mpaka siku ambayo Nuhu aliingia kwenye safina. 39 Hawakujua juu ya kilichokuwa kinaendelea mpaka mafuriko yalipowajia na kuwaangamiza wote.

Ndiyo itakavyokuwa Mwana wa Adamu atakapokuja. 40 Wanaume wawili watakuwa wakifanya kazi shambani, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa. 41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

42 Hivyo iweni tayari daima. Hamjui siku ambayo Bwana wenu atarudi. 43 Mwenye nyumba angefanya nini ikiwa angejua wakati ambao mwizi atakuja? Mnajua angelikesha ili mwizi asivunje na kuingia. 44 Hivyo, ninyi nanyi iweni tayari. Mwana wa Adamu atakuja katika wakati msiomtarajia.

Watumishi Wema na Wabaya

(Mk 13:33-37; Lk 12:41-48)

45 Fikiria mtumishi aliyewekwa na bwana wake kuwapa chakula watumishi wake wengine katika muda uliopangwa. Ni kwa namna gani mtumishi huyo atajionyesha kuwa ni mwangalifu na mwaminifu? 46 Bwana wake atakaporudi na kumkuta anafanya kazi aliyompa, siku hiyo itakuwa siku ya furaha kwa mtumishi huyo. 47 Ninawaambia bila mashaka yoyote kuwa, bwana wake atamchagua mtumishi huyo awe msimamizi wa kila kitu anachomiliki yule Bwana.

48 Lakini nini kitatokea ikiwa mtumishi huyo ni mbaya na akadhani kuwa bwana wake hatarudi karibuni? 49 Ataanza kuwapiga watumishi wengine na kuanza kunywa na kula na walevi. 50 Ndipo bwana wake atakuja wakati asioutarajia, ambapo mtumishi hakujiandaa. 51 Bwana atamwadhibu mtumishi huyo na kumpeleka anakostahili kuwapo pamoja na watumishi wengine waliojifanya kuwa wema. Huko watalia na kusaga meno kwa maumivu.

Read full chapter

Footnotes

  1. 24:29 Tazama Isa 13:10; 34:4.
  2. 24:33 wakati Wakati ambao Yesu aliuzungumzia ni ule ambapo kitu muhimu kitatokea. Tazama Lk 21:31, pale ambapo Yesu anasema huu ni wakati wa Ufalme wa Mungu kutufikia.